Hali ya simanzi imetawala miongoni mwa wakazi wa Makete mjini mkoani
Njombe kufuatia utingo wa lori lililobeba skaveta kugongwa na lori hilo
hadi kufa papo hapo.
Tukio hilo limetokea jana majira ya saa 11:45 alfajiri wakati lori
hilo likipita kwenye eneo lililolundikwa vifusi kufuatia matengenezo ya
barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Akizungumza na eddy blog mkuu wa polisi wilaya ya Makete Bw. Alfred
Kasonde amemtaja marehemu kuwa ni Albert Mwalukasa (21) ambaye amegongwa
na lori hilo lenye namba za usajili T 489 BDW mali ya Timoth Mwalukasa
mkazi wa mkoa wa Mbeya.
Lori hilo lilikuwa likiendeshwa na Bw. Lewad Mekule ambaye kwa sasa
anashikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano zaidi na upelelezi tayari
umekamilika hivyo atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya mauaji
yanayomkabili.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia Maiti cha
hospitali ya wilaya ya Makete ukisubiri ndugu wa marehemu waliopo
mkoani Mbeya kufika kuuchukua kwa ajili ya taratibu za kumzika.
Baba mdogo wa marehemu aitwaye Allan Mwalukasa ambaye alikuwepo
kwenye lori hilo amesema hata yeye anashangaa kilichopelekea kifo cha
ndugu yake kimetokeaje.
"Nilikuwa mbele hapa naangalia sehemu ambayo kidogo ni nzuri kwa
ajili ya vifusi hapa ambavyo vimelundikwa barabarani ghafla nkashangaa
nimesikia kelele nyuma huko analia aaaaah nikashindwa kuelewa, kuja
kukimbia ninamkuta yupo chini ya gari, huyo ni mtoto wa kaka yangu
ambaye tumefuatana" amesema Mwalukasa.
Kwa upande wa wananchi waliofika eneo la tukio wamesema marehemu
alikuwa akimuongoza dereva namna ya kupitisha lori kwenye vifusi
vilivyolundikwa muda mrefu barabarani bila kusambazwa, lakini ghafla
aliteleza kwa kuwa alikuwa akipita juu ya vifusi hivyo ndipo alipogongwa
na kufariki papo hapo.
Wananchi hao wametupa lawama kutokana na vifusi hivyo kukaa muda
mrefu bila kusambazwa hali inayopelekea usumbufu kwa watumiaji wa
barabara hiyo, na hivi karibuni mwandishi wetu alizungumza na mkandarasi
wa ujenzi huo ambaye alisema amekwenda Morogoro kufuata vifaa vya
kumalilisha ujenzi huo.
Hata hivyo wameshauri barabara mbadala zilizojengwa na mkandarasi huyo zitumike ili kuepusha madhara zaidi.
0 comments:
Chapisha Maoni