JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU HATUA MBALIMBALI AMBAZO SERIKALI INAENDELEA KUCHUKUA KUFUATIA
TISHIO LA UGONJWA WA EBOLA NCHI ZA AFRIKA MAGHARIBI NA KATI
Mnamo
mwezi wa Machi 2014, Serikali ilipokea taarifa kutoka Shirika la Afya
Duniani (WHO) kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Ebola uliotokea katika nchi
za Afrika Magharibi. Ugonjwa huu ulianzia katika Nchi ya Guinea na
kusambaa katika nchi za Liberia, Siera Leone na Nigeria. Aidha Ugonjwa
huu umeshatolewa tarifa pia nchini Senegal na Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC). Hadi kufikia tarehe 18 Septemba 2014, dadi ya watu
waliothibitishwa kuambukizwa ugonjwa huu imefikia 5335 na vifo 2662
(CFR=48.9%).
Aidha, hadi kufikia tarehe 16 Septemba 2014, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) idadi ya wagonjwa imefikia 71 na vifo 40.
Hali hii
imepelekea Shirika la Afya Duniani (WHO) kuutangaza ugonjwa wa Ebola
kuwa janga la Dunia (Public Health Emegency of International Concern).
Ugonjwa
wa Ebola husababishwa na virusi vya Ebola. Virusi hivi vipo katika
kundi la Familia ya “Filovirus”. Kuna aina tano (5) za “species” za
virusi hivi yaani Bundibugyo, Côte d’Ivoire, Reston, Sudan na Zaïre.
Aidha inakadiriwa kuwa asilimia 25 hadi 90 ya waliopata maambukizo ya
ugonjwa huu, hufariki dunia. Mlipuko uilotokea nchi za Afrika Magharibi
umesababishwa na kirusi aina ya Zaire Kwa kawaida virusi hivi hubebwa na
popo na uambukizo wa kwanza kabla ya kuenea kwa binadamu huanzia kwa
wanyama hususan nyani na sokwe.
Binadamu
hupata uambukizo kupitia popo au kupitia wanyama (sokwe, nyani na swala
wa porini) ambao wameambukizwa au waliokufa wakati wa shghuli za
uwindaji. Mara binadamu anapopata uambukizo huu, anaweza kueneza kutoka
kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine kupitia njia zifuatazo;
kugusa damu au majimaji kutoka mwilini mwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo
kugusa maiti ya mtu au mzoga wa mnyama aliyekufa kutokana na ugonjwa huu.
Dalili za
awali ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuumwa
na kichwa, na kutokwa na vidonda kooni. Mara nyingi dalili hizi
hufuatiwa na kutapika, kuharisha,kutokwa na vipele vya ngozi, figo na
ini kushindwa kufanya kazi na kwa baadhi ya wagonjwa hutokwa damu ndani
na nje ya mwili. Kipindi kati ya kupata maambukizi mpaka kuonekana kwa
dalili za ugonjwa ni kati ya siku 2 hadi 21. Ugonjwa wa Ebola hauna Tiba
maalum wala chanjo. Hata hivyo mgonjwa anatibiwa kutegemeana na dalili
atakazokuwa nazo.
Hadi sasa
hakuna mgonjwa yoyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya
Ebola hapa nchini. Kumekuwa na tetesi za wagonjwa wanne (4) kutoka mkoa
wa Dar es salaam (2), mmoja (Nkasi) na mmoja (Geita) waliohisiwa kuwa na
ugonjwa wa Ebola, lakini vipimo vimethibitisha kuwa HAWANA UGONJWA HUO.
Kwa kuwa magonjwa hayatambui mipaka ya nchi, Serikali inaendelea
kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya Ugonjwa huu.
Hatua ambazo zinaendelea kuchukuliwa na Serikali ni pamoja na;
Uratibu:
Uratibu wa shughuli unasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu –Kitengo cha
Maafa. Aidha sekta ya afya ndio msimamizi wa wa ugonjwa huu kwa kuwa
maambukizi yako kwa binadamu. Kikosi kazi hukutana kila wiki siku ya
alhamisi kufanya tathmini ya hali ya ugonjwa katika nchi zilizoathirika
pamoja na mikakati iliyowekwa kitaifa. Vikao hivi vinasimamiwa na
viongozi wa ngazi za Juu ikiwemo mawaziri na vinajumuisha sekta
mbalimbali pamoja na wadau wa maendeleo. Mpango kazi umeendelea
kuboreshwa kufuatia mwongozo wa Shirika la Afya Duniani na kusambazwa
mikoani na wilayani. AIdha kiasi cha Tshs500,000,000 zimeshapokelewa
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na zinategemea kutekeleza yafuatayo;
Uimarishaji
wa sehemu ya kuwahudumia wagonjwa kwa mkoa wa Dar es salaam “Isolation
Unit” iliyopo katika eneo la hospital ya Temeke
Uendelezaji
wa usambazaji wa elimu, tarifa na habari kwa jamii kutumia mabango,
vipeperushi, radio, runinga, na meseji kwa njia ya simu
Ununuaji wa vifaa cha kupimia joto (Thermoscanners) kwenye maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege
Mafunzo kwa watumishi wa afya
Katika
uratibu vilevile, mnamo tarehe 9 Septemba 2014, Mheshimiwa Rais, Dkt
Jakaya Mrisho Kikwete alishiriki katika ukaguzi wa hatua zilizofanyika
na kufanya majadiliano na kikosi kazi ya namna ya kuboresha baadhi ya
mikakati iliyowekwa.
Aidha
viongozi wa juu wa Serikali wakiwemo makatibu wakuu na mawaziri wamekuwa
wanahudhuria mikutano mbalimbali ya kanda (Regional body meetings) kama
mikutano ya “Africa Union”, “SADC” na “EAC” ikiwa ni katika kupanga na
kuweka maazimio ya pamoja kudhibiti ugonjwa huu barani Afrika
Kuimarisha
ufuatitiaji katika viwanja vya ndege na mipakani: Serikali imeshaweka
vifaa vya kuchunguza wageni wanaoingia nchini “Walk through
Thermoscanners” kwenye viwanja vya ndege na mikapani kama uwanja wa
ndege wa Julius Nyerere, KIA, Mbeya, na Mwanza, na mipaka ya Namanga,
Kabanga na Zanzibar. Aidha katika maeneo ya mipaka ya Holili, Sirari,
Kasumulo, Mutukula na Pemba pia zimewekwa “Hand Thermoscanners”. Vifaa
hivi si kwa ajili ya kutambua iwapo mgonjwa ana ugonjwa wa Ebola bali
vinalenga kurahisisha utambuzi wa wasafiri watakaokuwa wanarudi na kuwa
na dalili za mwanzo ambayo ni Homa. Fomu maalum za kuhoji wasafiri
zinaendelea kutumika kwa wasafiri wanaobainika kuwa na ugonjwa huu.
Orodha ya abiria kwenye ndege (Passenger manifest) pia inaendelea
kutumika ikishirikisha maafisa wa Uhamiaji lengo likiwa ni kutambua kwa
urahisi wasafiri ambao wamepitia nchi zilizoathirika. Ili wasafiri
waweze kutambua kuwa kutakuwa na utarabu tajwa, mabango ya maelekezo
yameandaliwa kuwekwa kwenye maeneo ya kuwasili (Arrival) na kutokea
(Departure).
Utoaji wa
Elimu, Taarifa na Habari kwa jamii: Serikali imeendelea kutoa elimu
kupitia njia nyingine zaidi ya redio na runinga. Aidha waandishi wa
Habari walipewa semina kuhusu ugonjwa wa Ebola.. Vilevile, Asasi ya
TAYOA imekubali kuchangia utumiaji wa mpango wa “toll free numbers”
ambazo tayari zinatumika kwa ugonjwa wa UKIMWI na zitaanza kutumika pia
kwa ugonjwa wa Ebola ili jamii iweze kupata ufafanuzi zaidi ya ugonjwa
huu pindi itakapohitajika. Namba hiyo ya “Toll free number” ni 117 na
itaanza kutumika punde kuanzia saa sita mchana na saa sita usiku kupata
taarifa za ugonjwa wa Ebola.
Ufuatiliaji
wa magonjwa katika vituo vya afya: Kupitia ofisi ya Waziri Mkuu
TAMISEMI, Serikali imetoa maagizo kwa Makatibu Tawala na Waganga wakuu
wa mikoa wakati wa mkutano wa Waganga wakuu Septemba 2014, kuandaa
mpango kazi wa namna ya kukabiliana na ugonjwa huu na kuandaa sehemu ya
kutolea matibabu kwa wagonjwa watakaohisiwa kuwa na ugonjwa huu
(Isolation Units). Kikosi kazi kitafanya ufuatiliaji wa karibu wa Agizo
katika mikoa na wilaya.
Mafunzo
kwa watumishi wa Afya: Mafunzo yameendelea kutolewa kwa watumishi wa
viwanja vya ndege, mipakani na vituo vya kutoa huduma za afya pamoja na
Maafisa wa Idara ya Uhamiaji yalifanyika Agosti 2014 kwa kushirikiana na
ufadhili wa Shirika la Afya Duniani (WHO). Idadi ya watumishi
waliokwisha kupata mafunzo ni;
100 kutoka Dar es salaam
45 kutoka mkoani Arusha, Kagera, Rukwa, Mwanza, Kilimanjaro, na Kigoma na Zanzibar
Wizara
pia imepata nafasi ya kupeleka watumishi watatu (3) nchini Congo
Brazaville; watano (5) nchini Afrika kusini na wanne (4) nchini Uganda
kwa lengo la kujifunza kutoka nchi nyingine na pia kuboresha mpango
mkakati ambao umeshaandaliwa.
Wizara kwa kushirikana na TAMISEMI inaendelea kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya kuanzia ngazi ya chini mpaka ya juu.
Vifaa vya
kujikinga (Personal Protective Gears): Vifaa kinga vipo vya kutosha kwa
ajili ya matumizi kwa watoa huduma kwa wagonjwa. Jumla ya vifaa vya
kujikinga (Personal Protective Gears) 12,750 vimenunuliwa na kuanza
kusambazwa katika hospital za wilaya, mkoa na rufaa. Tunatarajia kupata
vifaa vingine kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirka la Afya la
Marekani (CDC). Aidha idadi hii itaongezwa kadiri ya mahitaji
yatakavyojitokeza.
Maeneo ya
kutolea huduma za afya kwa watakaobanika na ugonjwa: Wizara imebainisha
vituo vya kutolea huduma kwa mikoa yote endapo ugonjwa huu utatokea
hapa nchini.. Katika mkoa wa Dar es salaam, Temeke Isolation Unit
limetengwa kama eneo la kuwahudumia wagonjwa wa Ebola kwa mkoa huu.
Sehemu hii inaendelea kuboreshwa kwa kuzingatia vigezo maalum ili iweze
kukidhi matibabu ya Ugonjwa huu. Aidha SUMA JKT wamepewa kazi ya
ukarabati wa majengo na kazi hii imeshaanza kufanyika.
Kuweka
mkakati wa namna ugonjwa huu utakavyoweza kutambulika mapema: Mipango ya
awali ni kutumia maabara ya KEMRI, Nairobi kwa sasa wakati uboreshaji
wa maabara zetu unaendelea ili kupata ithibati na kuweza kufanya
utambuzi hapa nchini.
Wizara
inaendelea kuwasiliana na wadau mbalimbali ikiwemo wadau wa maendeleo
ili kuweza kupata msaada wa mahitaji mbalimbali kama yalivyoainishwa
kwenye mpango wa dharura wa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola. Aidha
mkutano wa pamoja wa wadau unaandaliwa mwezi Septemba 2014 ambapo
utasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu..
Kupeleka
wataalamu wa afya katika nchi zilizoathirika. Serikali itapeleka
wataalam 9 katika nchi zilizoathirika ikiwa ni kwa ajili ya kujenga
uwezo wa wataalam wetu hapa nchini. . Aidha upelekaji wa wataalam hawa
unalenga pia kuimarisha dhana ya kusaidiana kama ambavyo Baba wa Taifa
alivyokuwa anafanya miaka ya nyuma wakati wa kudai uhuru katika Bara la
Afrika.
Hitimisho
Wizara
inapenda kuwatoa hofu wananchi kuwa hadi sasa hakuna mgonjwa yeyote
aliyethibitishwa kuwa na virusi vya ugonjwa Ebola hapa nchini.
Wananchi
wanashauriwa kutokuwa na hofu ila kuendelea kuchukua tahadhari. Ugonjwa
wa Ebola unaweza kuzuilika. Njia kuu za kujikinga na ugonjwa huu ni:-
Kuepuka
kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho, kinyesi, machozi na
majimaji mengine yanayotoka mwilini kwa mgonjwa mwenye dalili za
ugonjwa wa Ebola Kuhakikisha kuwa unanawa mikono kwa maji na sabuni au
kwa kutumia kwa dawa ya kuua vijidudu (hand sanitizers)
Kuepuka
kushughulikia maiti ya mtu aliyekufa akiwa na dalili za ugonjwa wa
Ebola; badala yake watoe taarifa kwa uongozi wa kituo cha kutolea huduma
za Afya kwa ushauri. Wataalam watasimamia maziko ikiwa itatokea.
Wananchi waepuke mila na desturi zinazoweza kuchelewesha kupata huduma muhimu na kuzidi kueneza ugonjwa wa Ebola.
Kutoa
taarifa mapema kwa viongozi wa Serikali na watoa huduma za Afya katika
ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola.
Kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za Afya pale mtu anapohisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.
Wizara
itaendelea na utaratibu wa kupashana habari na taarifa hizi kila wiki
kuanzia leo tarehe 18.9.2014 ikiwa ni lengo la kushirikisha jamii ili
iweze kushiriki katka utekelezaji wa mikakati ya kudhibiti ugonjwa huu
usiingie nchini.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Tarehe 18 Septemba 2014.
0 comments:
Chapisha Maoni