WANANCHI wa Jimbo la Ulanga Magharibi mkoani Morogoro, wamemuomba Rais Jakaya Kikwete kutimiza ahadi yake ya uchaguzi za mwaka 2010, ya kuwapatia wilaya mpya kwa mipaka ya kimajimbo.
Walisema kuwa kwa hali inavyokwena sasa wakati huu muda ya Rais Kikwete ukielekea ukingoni, baadhi ya watendaji na viongozi wa kiserikali wanakwamisha mchakato huo kwa makusudi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mikutano ya hadhara kwenye vijiji na makao makuu ya tarafa nne za wilaya hiyo za Lupiro, Mtimbira, Malinyi na Ngoheranga, baadhi ya wananchi hao, walidai kushangazwa na ugumu unaojitokeza katika upatikanaji wa wilaya mpya wakati walishamuomba Rais na akaahidi kuwapatia.
Kwa nyakati tofauti wananchi hao walibainisha umuhimu wa wilaya mpya ili kusogeza huduma za kijamii na kiuchumi karibu, huku wale wa Minepa wakimtuhumu diwani wao Athumani Kapati kuwashawishi kukubali Lupiro iende Ulanga Mashariki.
Wananchi hao walidai kuwa wana hofu ya mchakato huo umeanza kuingiliwa na mbunge wa Ulanga Mashariki, Celina Kombani ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) kwamba amekuwa akifanya kampeni za kuwashawishi wataalamu wa wilaya na mkoa huku akiwataka wananchi kukubali tarafa ya Lupiro ihamishiwe Ulanga Mashariki kwa maslahi yake binafsi.
Walidai kiongozi huyo huwaeleza watu wa Malinyi kuwa iwapo Lupiro itaaondoka katika jimbo hilo, makao makuu yatakuwa ni Malinyi, na vivyo hivyo akiwaeleza wananchi wa Mtimbira kuwa wakifikia maamuzi hayo, basi makao makuu ya wilaya yatakuwa katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa wananchi hao, hofu yao ilizidi zaidi baada ya ziara ya karibuni wilayani humo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia aliyewaeleza kuwa bado ni ndoto kwa Ulanga kugawanywa iwapo kutaendelea kuwepo masharti yanayokinzana na taratibu, kanuni na sheria za upatikanaji wa wilaya mpya.
0 comments:
Chapisha Maoni