Text Widget

Recent Posts

Agosti 08, 2014

ATC yalipisha kwa dola



Ofisi ya Shirika la Ndege Tanzania (ATC)KINYUME na agizo la Serikali la kutaka taasisi zake zisitoze malipo kwa dola ila kulinda thamani ya shilingi yake, Shirika la Ndege Tanzania (ATC), limekiuka kwa kuwalipisha kwa dola wapangaji wake wanaoegesha magari yao maegesho ya shirika hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Julai 24 mwaka huu, iliyosainiwa na Ofisa Mkuu (Utawala na Rasilimali Watu), Eliezer Mwale, wapangaji wote wanaarifiwa kuwa kuanzia Agosti 1, 2014, kila mmoja atapaswa kulipia dola 40 kwa mwezi kwa kila gari litakalokuwa limeegeshwa.
“Utaratibu huu hautawahusu wateja watakofika kupata huduma kwa wapangaji au ATC wakiwa na magari ambayo yatakuwepo kwa muda mfupi na kuondoka. Wateja hao watakuwa na eneo maalum la kuegesha magari yao na kupewa kadi maalum,” ilisomeka taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, malipo hayo yatafanyika wiki ya kwanza ya kila mwezi na kwamba endapo mpangaji atalaza gari lake, atalipia dola 20 zaidi kwa ajili ya huduma hiyo.
Wakizungumza na Tanzania Daima, kwa sharti la kuhifadhiwa majina yao, baadhi ya wapangaji walieleza kushangazwa na shirika hilo kulazimisha walipe kwa dola, wakati serikali ilikwishapiga marufuku taasisi zake kufanya hivyo kama mkakati wa kulinda thamani ya shilingi yake.
“Kulipa kwa dola tunagharamika zaidi, na baadhi yetu walijaribu kulipa kwa shilingi wakakataliwa. Hatuelewi kuna ajenda gani ndani yake, maana inachekesha kuona tiketi ambayo inauzwa bei kubwa abiria wanalipa kwa shilingi lakini maegesho ya magari tulalazimishwa kulipa kwa dola? alihoji mmoja wao.
Mkurugenzi Mkuu wa ATC, Milton Lazaro, hakupokea simu yake ili kufafanua mkanganyiko huo na hata alipotafutwa Mkurugenzi wa Biashara wa shirika hilo, Juma Boma, alisema atafutwe mtu anayehusika bila kumtaja.

0 comments:

Chapisha Maoni