Mkandarasi
mkuu anaeshughulikia mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es
Salaam, Strabag International ametangaza kufungwa kwa muda kipande cha
barabara ya Mandela hadi makutano ya Ubungo Mataa kuanzia leo.
Akiongea
jana na waandishi wa habari, Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Bw. Yahya
Mkumba alisema kipande cha barabara ya Mandela kuanzia makutano ya
barabara ya morogoro upande wa kushoto uelekeo wa Tabata kuanzia ubungo
mataa hadi darajani patafungwa.
Kipande
hicho kitafungwa kuanzia tarehe 25/08/2014 mpaka tarehe 30/08/2014 ili
kupisha ujenzi wa kipande cha barabara hiyo na hivyo kuwalazimu
watumiaji wa barabara hiyo kutumia barabara ya upande mmoja.
Akifafanua
zaidi ofisa uhusiano huyo alisema magari yatakayokuwa yanatokea Mwenge,
Kimara na Shekilango yatalazimika kutumia barabara ya upande wa kulia
ambayo pia itakuwa ikitumika na magari yanayo toka Tabata kuelekea
Ubungo.
“Tunaomba radhi kwa usumbufu utakaotokea,” alisema Bw. Mkumba.
Mradi wa Mabasi yaendayo haraka unatarajiwa kuondoa adha ya foleni katika jiji hilo na kuleta ufanisi wa usafiri.
Awamu ya kwanza ya mradi huo inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwaka huu.
0 comments:
Chapisha Maoni