Text Widget

Recent Posts

Oktoba 24, 2013

HAKIMU WA MWANZO AKATALIWA HADHALANI NA WANANCHI

 




 

 
Na Moses Augustine,Chato,0764207952

WANANCHI wa kijiji cha Mapinduzi kata ya Buseresere wilayani Chato Mkoani Geita, wamemkataa hadharani hakimu wa mahakama ya mwanzo wa kata hiyo, Mossy Soro, kwa madai ya kuwachonganisha na serikali yao.


Hatua hiyo inafuatia baada ya mahakama hiyo kumhukumu kwenda jela miaka 2 na akitoka kulipa fidia ya shilingi milioni 2.4 au kulipa faini ya shilingi 500,000 mwenyekiti wa kitongoji cha Mapinduzi,Theonest Laurent, aliyeshitakiwa na Mussa Husseini kwa madai ya kuharibu miti 62 iliyokuwa kwenye shamba lake.

Mbali na hilo,wamedai kuna hatari ya kutokea uvunjifu wa amani iwapo hakimu huyo, Mossy Soro,ataendelea kusikiliza mashauri ya kesi za wananchi wa kijiji hicho,na kwamba mwarobaini wake ni serikali kumwondoa eneo hilo na kupeleka mwingine mwenye maadili ya utumishi wa kimahakama.

Hukumu hiyo ilitolewa septemba 23 mwaka huu na hakimu wa mahakama hiyo,ambaye alisema kutokana na ushahidi uliotolewa na pande zote mbili mahakama ilijilidhisha kuwa mlalamikiwa ambaye ni mwenyekiti wa kitongoji hicho, alithibitika kuwa na hatia na kwamba hukumu hiyo iwe fundisho kwa viongozi wengine wenye kutumia madaraka yao vibaya.

Wakiwa katika mkutano wa hadhara wa kijiji cha Mapinduzi wananchi hao walisema hawakubaliani na maamuzi ya mahakama hiyo yaliyotolewa na mheshimiwa Soro kutokana na eneo lililodaiwa kuwa na miti hiyo kutokuwa na miche hiyo tangu mlalamikaji alipoingia kijijini hapo.


Aidha walidai kushangazwa na hatua hiyo kutokana na eneo hilo lililodaiwa kuwa na miti 62 kuwa na ukubwa wa meta 10 pekee na kwamba hatua iliyotumiwa na mwenyekiti huyo ilitokana na maamuzi halali ya mkutano wa kijiji ulioazimia kuchongwa barabara za mitaa ili kuvutia uwekezaji kwenye kijiji hicho.

Walisema hakimu huyo pamoja na mlalamikaji wa eneo hilo walilenga kupinga maendeleo ya kijijji kutokana na uamuzi wa kutengeneza barabara kuzingatia taratibu na kanuni zote ikiwemo maazimio ya mkutano mkuu wa kijiji uliolidhia utengenezwaji wa barabara za mitaa.

Jumapili Amri,Deograthias Julius na mwl,Komandoo Alex walidai kushangazwa na maamuzi yaliyotolewa na hakimu huyo kwa kuwa eneo hilo wanalifahamu kwa miaka mingi na kwamba hapakuwa na miti ya aina yoyote, aidha uamuzi huo ulitokana na kiongozi kutafuta maslahi binafsi ili kupindisha ukweli.

Kutokana na hali hiyo walidai hawana imani na hakimu huyo,huku wakitishia kwenda kuifunga mahakama hiyo mpaka hapo serikali itakapo peleka mtu mwingine kusimamia mashauri ya wananchi wa kijiji na kata hiyo.

Diwani wa kata ya Buseresere, Crespen Kagoma, alisema hakimu huyo amekuwa akilenga kuwagombanisha  wananchi na serikali yao kutokana na maamuzi halali yaliyopitishwa na mkutano mkuu wa kijiji kuyapuuza na hata kuwakataa mashahidi wa upande wa mlalamikiwa kutoa utetezi wao katika kesi hiyo.

Kagoma alisema wananchi hao kwa pamoja wameridhia kumkataa hakimu huyo na kwamba wataiomba mahakama ya wilaya ya chato kupanga hakimu mwingine atakaye sikiliza mashauri ya wananchi wa kata hiyo tofauti na aliyepo sasa.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji hicho, Shaaban Hugo,alisema anaungana na maamuzi yaliyotolewa na wananchi hao kwa kuwa maamuzi ya hakimu yalilenga kuzorotesha maendeleo ya kijiji hicho ambacho kinakabiliwa na changamoto nyingi za miundombinu ya umeme,maji na barabara.

Alipotafutwa na gazeti hili ili kujibu tuhuma dhidi yake,Hakimu wa mahakama hiyo alidai kuwa yeye siyo msemaji wa mahakama na kwamba kama kuna malalamiko dhidi ya mahakama wanatakiwa kuwasiliana na viongozi waliojuu yake.

Hata hivyo baada ya Gazeti hili kumwomba kueleza iwapo anatambua kama kuna malalamiko dhidi yake aliamua kukata simu na hata alipotafutwa hakupatikana tena.

Kwa mujibu wa sheria za nchi, mahakama ya mwanzo haina uwezo wa kutoza faini inayozidi shilingi laki 200,000 au kumfunga mtu jela zaidi ya miezi 12 vinginevyo hukumu hiyo lazima ithibitishwe na hakimu wa wilaya mfawidhi kwaajili ya uthibitisho wa adhabu hiyo.

Hivyo kifungo kilichotolewa na hakimu huyo kina leta utata mbele ya uso wa sheria na kwamba serikali inapaswa kutazama kwa jicho la karibu juu ya watumishi kama hao ili kuondoa kero za kisheria kwa jamii.

                                 

0 comments:

Chapisha Maoni