UJENZI wa daraja la mto Rusumo linalounganisha nchi za Tanzania na Rwanda limeingia katika sura mpya baada ya Waziri wa Ujenzi Dk, John Magufuli kukosoa mlinganyo wa miundombinu iliyowekwa kati ya nchi hizo mbili.
Daraja hilo linalojengwa kwa ufadhili wa fedha za serikali ya Japan linadaiwa kuwa mkombozi kwa Uchumi wa wananchi wa Tanzania na Rwanda katika kukabiliana na soko la pamoja la nchi wanachama wa Afrika Mashariki.
Katika ziara hiyo ya ukaguzi wa ujenzi iliyofanywa na Waziri wa Ujenzi Dk Magufuli,mwakilishi wa Waziri wa Ujenzi nchini Rwanda pamoja na Balozi wa Japan nchini Tanzania Masaki Okada ilibaini baadhi ya mapungufu yaliyotokana na baadhi ya wataalamu wa serikali ya Tanzania kushindwa kutoa ushauri wenye manufaa kwa nchi yao.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Magufuli alisema licha ya ujenzi huo kugharimiwa na nchi ya Japan kwa aslimia 100, hapana mlinganyo sahihi wa miundombinu iliyojengwa kati ya upande wa Tanzania na Rwanda.
Miundombinu hiyo ni pamoja na wingi wa ofisi za idara mbalimbali za serikali,urefu wa barabara ya lami kufika kwenye daraja hilo,kituo kikubwa cha kupaki magari na mizigo, ikilinganishwa na Tanzania hatua inayohofiwa kupunguza Uchumi wa Tanzania kutokana na magari na mizigo mingi kushushwa Rwanda.
Aidha Dk, Magufuli aliipongeza Japan kukubali kufadhili zaidi ya Bilioni 35 kwaajili ya ujenzi huo ambao unatarajiwa kukamilika desemba 2014,
Awali akitoa taarifa ya ujenzi huo, Meneja wa Tanroad mkoa wa Kagera, John Kalupale,alisema ujenzi huo umekamilika kwa aslimia 60 ambapo upande wa Tanzania umetekelezwa kwa aslimia 25 huku Rwanda wakiwa wametekeleza kwa aslimia 35 na kwamba unafanyika chini ya kampuni ya Daiho Corparations ya nchini Japan.
Kwa upande wake Balozi wa Japan nchini Tanzania,aliwatupia lawama baadhi ya viongozi wa serikali ya Tanzania kushindwa kuishauri serikali yao mapema juu ya ujenzi wa daraja hilo kufuatia malalamiko ya kuwa nchi ya Rwanda ilipendelewa na kwamba walitakiwa kueleza tofauti hizo awali kabla ya utekelezaji wa kazi kuanza
Mwakilishi wa Waziri wa Ujenzi nchini Rwanda, Guy Kalisa,alisema ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili utasaidia Kuinu Uchumi kutokana muungano wa soko la pamoja la nchi wananchama wa Afrika Mashariki kwa kuwa mizigo mingi itapitia kwenye daraja la mto Rusumo.
|
0 comments:
Chapisha Maoni