Text Widget

Recent Posts

Agosti 13, 2014

HII NI TAARIFA KWA UMMA, UKAWA KUANDAMANA NCHI NZIMA

Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).MCHAKATO WA KATIBA MPYA NA YANAYOENDELEA BUNGE MAALUM LA KATIBA
Ndugu wanahabari
Sote tunaelewa kuwa kwa matakwa ya CCM, Bunge Maalum la Katiba (BMK) limeendelea kufanya vikao vyake mjini Dodoma kuanzia Agosti 5 mwaka huu, kinyume kabisa na matarajio ya Watanzania, ambao kupitia fursa mbalimbali wamepaza sauti zao wakisisitiza maridhiano na mwafaka wa kitaifa kutangulizwa mbele badala ya maslahi ya watawala.
Tukiwa viongozi wa kisiasa ambao ni sehemu ya uongozi ndani ya jamii, wenye wajibu wa kuwa na maono chanya na muhimu kwa taifa letu, tumeendelea kufuatilia kwa karibu namna mchakato wa Katiba Mpya unavyoendelea kunajisiwa kupitia vikao hivyo vya BMK linaloendelea mjini Dodoma, likitumia rasilimali za taifa, zikiwemo kodi za Watanzania wanyonge, kujadili vitu visivyotokana na wananchi.

Mtu yeyote makini ataweza kubaini kuwa kwa namna mchakato wa Katiba Mpya unavyopelekwa au unavyokwenda kwa sasa ni matokeo ya kukosekana kwa uongozi wa kisiasa kwa Chama kinachoongoza Serikali, CCM.

Kuna ombwe kubwa la uongozi wa kisiasa katika jambo hili. Ni kama vile mchakato unajiendea tu wenyewe bila mwongozo wowote kutoka kwa watu walioko madarakani ambao wananchi walitarajia wangetumia mamlaka yao ya dhamana ya uongozi ili taifa lipite salama katika wakati huu mgumu na tupate Katiba Mpya na bora.

Vipo viashiria vingi tu vinavyoweka wazi hali hiyo ya ombwe la uongozi wa kisiasa katika mchakato huu wa kisiasa, ikiwa ni pamoja na kauli kinzani za viongozi wa Serikali na CCM yenyewe. 
Wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda akizungumza kama vile kunahitajika mazungumzo zaidi na kwamba suala la muundo wa serikali lilipaswa kupigiwa kura kabla, Mwenyekiti wa BMK anaendelea kuongoza bunge kama vile mchakato ni mali binafsi ya CCM na walioko madarakani.

Wakati baadhi ya viongozi wa Serikali ya CCM wakitoa kauli za kuhitaji kuwa makini na taratibu za kuendesha mchakato huu chama chao kinatoa kauli za kuzidi kuharamisha na kutia najisi mchakato mzima. Mchakato unakwama, nchi inayumba, Watanzania wako katika sintofahamu kwa sababu tu tumekosa uongozi wa kisiasa katika jambo hili.

Kiashiria kingine cha pengo hilo la uongozi wa kisiasa ambacho kwa kweli kwetu sisi kimetusikitisha zaidi kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kuendelea na ‘hamsini zake’ kama vile nchi haina tatizo lolote. 

Yaani wakati nchi na wananchi wako katika sintofahamu ya hatma ya Katiba Mpya itakayoweka misingi ya wao kujitawala na kuongozwa watakavyo, makundi mbalimbali yakipaza sauti zao, mataifa mengine yakituangalia kwa makini na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wakifuatilia mchakato, Rais Kikwete anapata muda wa kutembelea ranch ya Rais Mstaafu wa Marekani George Bush! 

Wakati Rais Kikwete akiendelea kutalii dunia, wenzake wako mjini Dodoma wakichukua posho kwa kazi ambayo wananchi hawajui wanaifanya kwa maslahi ya nani!

Kwa ujumla mambo yote yanayoendelea sasa katika mchakato huu ni matokeo ya ombwe hilo kama tulivyosema. 

Inaonesha kuwa CCM wamelewa madaraka na viongozi wanaona dhamana ya uongozi iko juu ya wananchi hivyo hawajali umuhimu na nafasi ya mamlaka ya wananchi katika kuamua mstakabali wa taifa lao kwa ajili ya kizazi cha sasa na kuweka msingi wa vizazi vingi vijavyo.
Hivyo leo tungependa kuzungumza tena kuhusu Rasimu ya Katiba na mchakato wenyewe hapa ulipokwama;

Tunapenda kusema wazi kuwa tumeshangazwa sana na kitendo cha CCM na Serikali yake kulazimisha kuendelea kwa Bunge Maalum la Katiba Mpya, tena kwa mtindo ule ule wa kunajisi na kupuuza maoni ya wananchi yaliyomo kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya kama yalivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Wamefanya hivyo pasi na kujali kilio cha wananchi kinachopazwa kutoka kila kona ya nchi, ambapo Watanzania mmoja mmoja na katika makundi mbalimbali wametaka maoni yao yazingatiwe kwa kujadiliwa, kuboreshwa na kisha kupitishwa na Bunge Maalum la Katiba kabla wao hawajayapigia kura ya maoni kwa ajili ya kuipitisha au kuikataa Rasimu ya Katiba Mpya.

Wajumbe wanaotokana na CCM pamoja na makada wengine wapatao 166 wa chama hicho ambao waliteuliwa kuingia kwenye bunge hilo kusimamia maslahi ya CCM kupitia kundi la wajumbe 201, wameamua bila haya mbele ya umma si tu kupuuza rasimu iliyotokana na maoni ya wananchi bali sasa wameamua kuingiza mambo yao waliyodhamiria tangu mwanzo kwa kadri ya maamuzi na maelekezo ya vikao vya chama hicho vikiongozwa na Mwenyekiti wao Jakaya Kikwete.

Bila kujali wala kuguswa na miito ya Watanzania mbalimbali wanaotaka jambo hili liongozwe na maridhiano kwa ajili ya mwafaka wa kitaifa badala ya kuweka matamanio ya watawala mbele, CCM na mawakala wao katika mchakato huu wameendelea pia kufuja na kutumia vibaya fedha za wananchi kupitia Bunge Maalum la Katiba kwa kujadili na kuingiza vitu visivyokuwemo au visiyotakiwa kuwa sehemu ya rasimu hii iliyopo sasa.

Hali hiyo imefanyika kwa namna kadhaa ikiwa ni pamoja na kutofuata sheria inayosimamia mchakato mzima, kubadili kanuni za uendeshaji wa BMK hasa katika taratibu za kujadili na kupitisha ibara na kubwa zaidi kuingiza masuala ya Tanganyika kwenye Rasimu ya Katiba ya Muungano.

Kimsingi masuala wanayoyajadili na kuyachomeka kinyemela kwenye Rasimu ya Pili ya Warioba, mathalan masuala ya Ardhi, Elimu, Maji, Kilimo, Uvuvi, Mifugo, Serikali za Mitaa nk ni masuala yanayopaswa kuandikwa kwa kina ndani ya Katiba ya Tanganyika na siyo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ni vyema kukumbuka kuwa Zanzibar walijadili wenyewe mambo Yao ya Ndani na kutengeneza Katiba yao na hatuoni mantiki ya kuruhusu Wajumbe toka Zanzibar kujadili na kuamua mambo ya Tanganyika. BMK haina Sifa ya kujadili yasiyo ya Muungano.

Hivyo tofauti na wanavyotaka kujionesha katika jamii, CCM kupitia BMK wameamua kupindua kabisa rasimu nzima na kuweka maazimio ya vikao vyao kuwa ndiyo Katiba ya Tanzania. Jambo hili haliwezi kukubalika.

Kutokana na uchakachuaji huo wa Katiba Mpya unaoendelea kufanywa na CCM kupitia BMK, UKAWA tumefikia maamuzi yafuatayo;

· Tunamtaka Rais Jakaya Kikwete asitishe shughuli za BMK mara moja lisiendelee kuvuruga
na kuharibu mchakato wa Katiba Mpya na kuiweka nchi katika sintofahamu juu ya jambo hili
nyeti;
· Tunamtaka Rais Kikwete asitishe BMK ili lisiendelee kufuja fedha za Watanzania maskini
wanaopigania Katiba Mpya iwapatie matumaini ya kuongozwa na kujitawala wanavyotaka.

· Tunamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum
kwenye matumizi ya fedha za BMK ambayo kuanzia Bunge la Bajeti lililopita tumebainisha
wazi kuwa yana uvundo mkubwa wa ufisadi na hayana maelezo sahihi.

· Iwapo Rais Kikwete atashindwa kutumia mamlaka yake kusitisha BMK na hivyo likaendelea
kinyume cha matakwa na maslahi ya wananchi kama lilivyofanya awali na linavyofanya sasa,
UKAWA tutawaongoza Watanzania kupaza sauti zaidi kupinga najisi inayotiwa kwenye maoni
yao, kupitia maandamano na mikutano ya hadhara nchi nzima.


Asanteni kwa kutusikiliza.


Prof. Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti CUF


Freeman Aikaeli Mbowe
Mwenyekiti CHADEMA


James Francis Mbatia
Mwenyekiti NCCR Mageuzi


Wilbrod Peter Slaa
Kny Makatibu Wakuu, UKAWA.

0 comments:

Chapisha Maoni