Frank Nyalusi Mwenyekiti wa Chadema Iringa Mjini |
Kama kawaida salamu za chama hicho za Peopleziii zilisika |
Mlemavu huyo aliuliza swali katika mkutano huo akitaka kujua kati ya Samwel Sitta na Rais jakaya Kikwete ni nani ana madaraka makubwa zaidi kuhusu mchakato wa Katiba |
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Iringa Mjini, kimetangaza kufanya maandamano ya amani kesho Jumatatu ikiwa ni hatua ya kuitikia wito wa mwenyekiti wao, Freeman Mbowe wa kufanya maandamano hayo nchi nzima kushinikiza kusitishwa kwa Bunge la Katiba.
Mwenyekiti wa Chadema wa Iringa Mjin, Frank Nyalusi alitoa tangazo hilo jana katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika katika mtaa wenye machinga wengi maarufu kama Magari Mabovu, Kitanzani.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na vijana kadhaa huku ukiwa umezungukwa na askari Polisi kila kona, Nyalusi alisema “wapende wasipende, kesho tutafanya maandamano, tunaomba Polisi washiriki kulinda usalama wetu, kwani maandamano hayo yatakuwa ya amani.”
Alisema maandamano hayo yanalenga kupeleka ujumbe wa kusitishwa kwa mchakato wa bunge hilo kwa kuwa hauna maridhiano na fedha zitakazonusurika zitumike katika shughuli zingine za kijamii.
“Hatuwezi kupata Katiba kwa staili hiyo, tumemuomba Rais asitishe mchakato huo lakini tumepuuzwa na sasa tunadhani ni zamu ya watanzania wote kupaza sauti zao ili bunge hilo lisitishwe,” alisema.
Alipoulizwa baadaye maandamano hayo yataanzia wapi, Nyalusi hakuwa tayari kutaja ni eneo gani yataanzia kwa kile alichosema hawataki wapinzani wao wajue.
Kabla ya kutangazwa kwa maandamano hayo ya kesho jumatatu, jeshi la Polisi liliripotiwa na chama hicho kuwazuia kufanya maandamano kama hayo Jumamosi iliyopita.
Badala yake kwa mujibu wa Nyalusi, jeshi hilo liliwaruhusu kufanya mkutano wa hadhara katika eneo hilo la Magari Mabovu.
Katika mahojiano na gazeti hili, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Ramadhani Mungi alisema jeshi lake halijapokea maombi ya maandamano hayo kutoka katika chama hicho.
Aliwataka wafuasi wa chama hicho kuzingatia sheria, taratibu na kanuni wakati kikipanga na kufanya mambo yake.
Akitoa ufafanuzi huo kwa njia ya simu, Mungi alisema; “nchi hii kama zilivyo nchi nyingine inaendeshwa kwa sheria. Kwahiyo watu binafsi, serikali, vyama vya siasa na wengine wote ni lazima wazingatie hilo.”
Alisema mji wa Iringa upo shwari na kwamba jeshi hilo limejipanga kikamilifu kukabiliana na hali yoyote ile itakayoonekana inataka kuhatarisha amani.
0 comments:
Chapisha Maoni