WHO yaonya kuwa vifo vinavyotokana na maambukizi ya Ebola vimetimia asilimia 70%
Idadi ya vifo vya wagonjwa wa Ebola imetimia asilimia 70% ya maambukizi ya ugonjwa huo .
Umoja wa Mataifa umeonya kwamba maambukizi ya Ebola huenda yakaongezeka
na kutimia 20,000 kufikia mwezi wa Novemba iwapo juhudi za kudhibiti
ugonjwa huo hazitaongezwa maradufu.
Marekani imeonya kwamba huenda maambukizi mabaya zaidi yakashuhudiwa
Januari mwakani ambapo maambukizi katika ukanda wa Afrika Magharibi
huenda yakagonga milioni 1.4.
Hata hivyo wadadisi wamesema makadirio hayo ya Marekani hayapendezi wala hayaonyeshi nia nzuri.
Mlipuko huo wa ugonjwa wa Ebola umesababisha vifo 2,800, visa vingi
vikiripotiwa katika mataifa ya Guinea, Liberia na Sierra Leone.
Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limesema mkurupuko wa ugonjwa huo ‘‘ulidhibitiwa vyema” nchini Nigeria na Senegal.
Wanasayansi wamesema hatua madhubuti za haraka zinafaa kuchukuliwa ili kuzuia kuenea zaidi kwa maambukizi ya ugonjwa wa Ebola.
Makisio mawili yanaonyesha kwamba maambukizi ya Ebola huenda yakaongezeka zaidi katika mataifa matatu yalioyoathirika zaidi.
WHO imeonya kuwa maambukizi huenda yakatimia 20,000 mwakani
Uchambuzi wa visa vilivyoripotiwa tayari unaonyesha kwamba idadi ya watu
wanaofariki imeongezeka mpaka asilimia 70% kutoka asilimia 50%.
Afisa wa WHO, bw. Christopher Dye ameonya kwamba ikiwa hatua za haraka
za kudhibiti ugonjwa huo hazitachukuliwa, maelfu ya visa hivi vitazidi
kuripotiwa kila juma katika mataifa hayo matatu.
Wakati huo huo wakfu wa Wellcome uimetangaza kwamba dawa za kuponya
ugonjwa huo zitafanyiwa majaribio kwa mara ya kwanza huko Afrika
Magharibi.
Moja ya dawa hizi inafahamika kama ZMapp ambayo tayari imepatiwa baadhi ya wagonjwa wa Ebola.
Dkt Peter Horby, kutoka Centre for Tropical Medicine and Global Health
iliyo katika chuo kikuu cha Oxford, amesema majaribio rasmi ya dawa hizo
yataanza Novemba, Afrika Magharibi.
0 comments:
Chapisha Maoni