Text Widget

Recent Posts

Agosti 06, 2014

Yanga OUT Kagame, Azam ndani


Katibu Mkuu wa Cecafa,Nicholas Musonye.
Timu ya soka ya Yanga imeondolewa rasmi kushiriki katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) yanayotarajiwa kufanyika Kigali, Rwanda kuanzia Ijumaa na nafasi yake imetwaliwa na mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Azam.

Yanga imeondolewa katika mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), kutokana na maamuzi yake ya kupeleka kikosi cha pili pamoja na kocha msaidizi, Mbrazil, Leonardo Neiva.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka Nairobi, Kenya, Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye, alisema Yanga ilifanya 'dharau' na shirikisho hilo halikuwa tayari kuruhusu hali hiyo iendelee.

Musonye alisema kuwa, tayari wamelipa taarifa Shirikisho la Soka nchini (TFF), mabadiliko hayo ya kuialika Azam ambayo pia imeshathibitisha kushiriki.

"Walifanya dharau, kikosi cha kwanza huambatana na kocha mkuu, kwanini Maximo (Marcio) abaki Dar es Salaam, ila maamuzi mengine tutayafanya tukifika Kigali," alisema Musonye.

Aliongeza kuwa, maandalizi mengine ya michuano hiyo yako katika hatua za mwisho na leo waamuzi watashiriki mtihani wa majaribio na wale watakaofaulu ndiyo watakaochezesha mashindano hayo yatakayomalizika Agosti 24, mwaka huu.

Alisema pia timu ya Coffee ya Ethiopia imejiondoa kushiriki michuano hiyo na nafasi yake kuchukuliwa na Adamma ya nchini humo wakati Atletico ya Burundi nayo itashiriki mashindano hayo.

Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa, alikiri kupokea taarifa kutoka Cecafa za kuondolewa kwa timu yao na Azam kupewa nafasi hiyo kwenye mashindano hayo.

"Ni kweli Cecafa imetujulisha kwamba itakwenda Azam badala ya Yanga, na wamefikia maamuzi hayo baada ya kutokubali Yanga ipeleke kikosi cha U-20, na Yanga nao walisisitiza kuipeleka timu hiyo, hivyo suluhu haikupatikana," alisema Mwesigwa.

Naye Katibu Mkuu wa Azam, Nassor Idrissa, alithibitisha timu yake kwenda kwenye mcihuano hiyo na kuongeza kwamba itaondoka nchini kesho mchana.

Aliwataja wachezaji 20 wa Azam watakaoshiriki michuano hiyo kuwa ni makipa; Aishi Manula, Mwadini Ally, mabeki Waziri Salum, Gadiel Michael, Shomary Kapombe, Abdallah Kheri, Aggrey Morris, Said Mourad na David Mwantika.

Viungo Kipre Balou kutoka Ivory Coast, Salum Abubakar, Mudathir Yahya, Himid Mao, Khamis Mcha ‘Vialli’, Farid Mussa na Joseph Peterson wa Haiti, wakati washambuliaji ni Didier Kavumbangu, Leonel Saint- Preux wa Haiti, Kipre Herman Tchetche wa Ivory Coast na John Bocco ‘Adebayor’.

Alimtaja Kocha Mkuu, Mcameroon, Joseph Marius Omog, Msaidizi Kali Ongala, kocha wa makipa Iddi Abubakar na Meneja, Jemadari Said, kuwa watakiongoza kikosi hicho kwenye michuano hiyo ya 40 tangu ilipoanza kuchezwa.

Azam iko Kundi A pamoja na wenyeji, Rayon Sport, Adamma ya Ethiopia, Atlabara ya Sudan Kusini na KMKM ya Zanzibar na itacheza mechi ya ufunguzi dhidi ya wenyeji Rayon Sport Uwanja wa Amahoro Agosti 8, mwaka huu, mchezo ambao utatanguliwa na mechi kati ya KMKM ya Zanzibar na Atlabara ya Sudan Kusini.

Kikosi cha Azam FC kitarudi tena dimbani, Agosti 10 kumenyana na jirani zao KMKM, kabla ya kucheza na Atlabara Agosti 12 na kukamilisha mechi za kundi lake, kwa kumenyana na Adamma ifikapo Agosti 16.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Chapisha Maoni