Na Neville Meena, Mwananchi
Dodoma. Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda amesema kama Serikali ingejua, ingeanza kwa kura za maoni ya
wananchi kuamua aina ya muungano wanaoutaka, kabla ya kuendelea na
mchakato wa Katiba.
“Tungejua kama hali ya aina hii itajitokeza, basi
tungeanza na kura ya maoni, tungewauliza wananchi kama wanautaka
muungano na kama ndiyo, basi uwe wa aina gani au serikali ngapi, mtu
angesema moja, mbili, tatu na kadhalika,” alisema Pinda jana kwenye
Viwanja vya Bunge mjini hapa.
Pinda alikuwa akijibu swali kuhusu hatima ya Bunge
Maalumu kutokana na wajumbe wa Bunge hilo ambao ni wanachama wa Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao hivyo wakishinikiza kile
walichokiita kujadiliwa kwa rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko
ya Katiba na siyo vinginevyo.
Miongoni mwa mambo ambayo yamezua mvutano mkubwa
ni muundo wa muungano wa serikali tatu uliopendekezwa na tume hiyo,
pendekezo ambalo linaungwa mkono na wajumbe wa Ukawa ambao wamesusa
Bunge, wakati upande mwingine wenye wabunge wengi wa CCM ukitaka muundo
wa serikali mbili uendelee.
Pinda alisema baada ya kupata majawabu ya aina ya
muundo wa muungano wanaoutaka wananchi kwa matokeo ya kura ya maoni,
basi ungekuwa wakati mwafaka wa kwenda kukusanya maoni ya wananchi
kuhusu mambo mengine katika Katiba.
“Lakini ndiyo hivyo, hatukuliwaza hili kwa hiyo
ndiyo tunapata taabu yote hii kwa sababu kama mnavyoona bado
hatujakubaliana, lakini wenzetu mpaka sasa hawajafika bungeni na mambo
kama hayo. Lakini bado tuna imani kwamba busara zitatumika ili mchakato
huu uwe wa maridhiano ya wote,” alisema Pinda na kuongeza:
“Katika kukusanya maoni ambayo tunayafanyia kazi
sasa, Tume ya Jaji Warioba (Joseph, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba) ilikusanya maoni mchanganyiko na utakuta pengine suala hili la
aina ya muungano halikuwa na mchango wa watu wengi.”
Alisema kama suala la aina ya muungano lingekuwa
limetafutiwa suluhu mapema, mambo mengine yote yangejadiliwa na
kuafikiwa kwa kuzingatia suala hilo ambalo linaonekana kuwa ni nguzo
muhimu ya Katiba.
Alisema jitihada bado zinaendelea ili kuwashawishi
Ukawa warejee bungeni na kwamba katika meza ya majadiliano hakuna
kinachoshindikana.
“Ninaamini kwamba hizi tofauti zinaweza kuondoka
kwa majadiliano, ni suala la kukubaliana kwamba ninyi chukua hiki na
sisi tunabaki na hiki na hapo mchakato unaendelea,” alisema.
Alisema imekuwa vyema kwamba kanuni za Bunge
Maalumu zimebadilishwa ili kuwezesha wajumbe kujadili maeneo mengine
katika Rasimu ya Katiba ambayo hayana utata na kwamba suala la muungano
linaweza kupewa fursa baadaye na wakati huo mwafaka unaweza kuwa
umepatikana.
0 comments:
Chapisha Maoni