Dar es Salaam. Hoteli ya Blue
Pearl ya jijini hapa imefungwa kwa muda usiojulikana baada ya mmiliki
wake kushindwa kulipa kodi ya pango ya Dola za Marekani 3,800,000 sawa
na Sh6 bilioni ambazo alilimbikiza kwa miaka mingi.
Jana mchana wafanyakazi wa Kampuni ya Udalali ya
Majembe walifika hotelini hapo na kuanza kutoa nje samani zilizokuwa
ndani ya hoteli na kuzipakia kwenye lori lililokuwa limepaki nje ya
lango kuu la kuingilia.
Hali hiyo ilisababisha kusitishwa kwa huduma
zilizokuwa zikitolewa na wateja waliambiwa watoke nje kwani hoteli hiyo
inafungwa na huduma hazitolewi tena.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Majembe, Seth
Motto alisema walifikia hatua hiyo baada ya uongozi wa Hoteli ya Ubungo
Plaza ambao ndiyo wamiliki wa jengo hilo kuwaomba wafanye kazi hiyo.
Alisema kazi yao ilikuwa ni kutekeleza ombi hilo
la kutoa samani zote zilizokuwa ndani ya hoteli ili mmiliki huyo aweze
kulipa deni.
“Tunafanya hivi kwa kufuata utaratibu wa kisheria.
Hata kama anasema mkataba wake haujaisha, lakini anatakiwa kufahamu
kwamba kitendo cha kushindwa kulipa kodi kimemfanya akasitishiwe mkataba
wake…lakini alipewa notice (taarifa) pia. “Wanaendesha hoteli kwa
gharama, kwa nini washindwe kulipa kodi,” aliuliza.
Awali, Mkurugenzi wa hoteli hiyo, Rustan Meran
alilalamika kuwa hakupewa taarifa mapema, akisema kitendo kilichofanywa
ni kinyume na utaratibu.
Hata hivyo, mkurugenzi huyo alidai kuwa bado
wanazungumza nao ili kupata mwafaka wa jambo hilo kwani mkataba wake
haujaisha. Alisema mkataba ni wa miaka 15 na imebaki miaka 7 kumaliza.
Naye Mwanasheria wa Majembe, Benard Kuwata alisema wanachofanya ni kuwasaidia Ubungo Plaza walipwe fedha zao.
0 comments:
Chapisha Maoni