Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba nusura wapigane baada ya kupishana kauli wakati wa mjadala wa ndani ya Kamati Namba Sita inayoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira.
Habari kutoka ndani ya kamati hiyo inayofanyia
vikao vyake katika moja ya kumbi za Dodoma Hoteli zinasema, mvutano huo
ulitokea Alhamisi iliyopita na kusababisha Wassira kusitisha kwa muda
kikao hicho, kisha kwenda kuwasuluhisha.
Jana, Wassira licha ya kukiri kutokea kwa mvutano
huo, alikanusha taarifa kwamba aliahirisha kikao hicho kwa ajili ya
kuwasuluhisha.
“Kupishana katika masuala haya makubwa ni jambo la
kawaida, hivyo mimi sidhani kama ni jambo linalopaswa kwenda mpaka
kwenye magazeti maana kila wakati hutokea tofauti hizi na ndiyo maana
sisi wenyeviti tupo ili kusimamia mijadala,” alisema Wassira na
kuongeza:
“Lakini kwamba eti hilo jambo lilisababisha kikao
kuahirishwa au kusitishwa hapana, kikao kiliendelea na kazi yake baada
ya hilo lililoleta na ubishani kumalizwa”.
Habari zilizolifikia gazeti hili zinasema mvutano
huo ulitokea wakati kamati hiyo ilipokuwa ikijadili Sura ya Nne na Tano,
hususan suala la uraia wa nchi mbili. Sura ya tano ndiyo inayozungumzia
masuala ya uraia.
“Sophia Simba yeye anataka uraia wa nchi mbili
wakati Werema alikuwa akisema hilo jambo haliwezekani kutokea kwa sasa,”
kilisema chanzo chetu.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mvutano huo uliendelea
baina ya viongozi hao na ndipo Jaji Werema aliposimama katika mchango
wake na kuhoji elimu ya Simba, hivyo kuamsha hasira za waziri huyo
ambaye pia alijibu mapigo.
“AG alipopewa nafasi ya kuzungumzia baada ya
mabishano ya muda alihoji shule (elimu) ya Simba kwamba amesoma shule
gani akimaanisha kwamba ni mgumu kuelewa, kwa hiyo waziri alikasirika na
yeye alianza kujibu mapigo,” kiliongeza chanzo hicho.
Baada ya kutokea mvutano huo, baadhi ya wajumbe
waliingilia kati kusitisha mzozo huo, ndipo Mwenyekiti Wassira
alipositisha kikao hicho kwa muda kisha kuwasuluhisha wahusika.
Walipotafutwa jana kwa nyakati tofauti kuzungumzia mzozo wao, Werema na Simba hawakuwa tayari kubainisha kilichotokea.
Werema alitaka aachwe apumzike na kwamba mambo ya kamati yaachwe kwenye kamati.
0 comments:
Chapisha Maoni