Na Suzan Mwillo, Mwananchi
Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa
Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe ameongeza
chumvi katika Mchakato wa Katiba kwa kueleza kuwa anaunga mkono msimamo
wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutorejea kwenye awamu ya pili ya
vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.
Kakobe pia alimtupia lawama Rais Jakaya Kikwete
akisema hotuba yake ya kufungua Bunge hilo ndiyo chanzo cha kuvuruga
mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya.
Kakobe ametoa kauli hiyo zikiwa zimepita takriban
siku tatu tangu Rais Kikwete alipotoa hotuba yake ya kila mwezi na
kujivua lawama hizo alizokuwa akitupiwa na watu wa kada mbalimbali.
“Naunga mkono Ukawa si kwa asilimia 100 bali
asilimia 150 kwa msimamo wao wa kususia vikao. Tena sitegemei kusikia
wamerejea bungeni, wakirejea watakuwa wamelogwa. Lazima wahakikishe
upungufu huo unafanyiwa kazi kabla ya kurejea kwenye awamu ya pili ya
vikao hivyo vilivyopangwa kuanza Agosti 5,” alisema.
Aliongeza: “Pengine kilichoonekana kuwa kibaya ni
jinsi nilivyozifasiri taarifa hizo na mapendekezo ya Tume. Sioni kosa
langu ni kutoa maoni kuhusu baadhi ya vipengele vya rasimu kwa sababu
imetolewa hadharani kwa watu kuijadili. Mimi kama raia ninayo haki ya
kufanya hivyo kama wafanyavyo wengine,” alisema Kikwete kwenye hotuba
hiyo.
Hata hivyo, jana Kakobe aliyezungumza kwenye
maadhimisho ya miaka 25 ya Kanisa la FGBF alisema kuwa anapingana na
utetezi huo kwani hauna hoja ya msingi kwani alishavuruga mchakato huo
tangu awali.
“Hotuba yake ya kufungua Bunge hilo ndiyo
iliyoharibu mambo yote hadi sasa tumefika katika hali hii.Anafanya hivyo
akiwa na dhamira ya kuvuruga mchakato huo ili usiendelee kwa kuhofia
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuanguka katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Mapendekezo ya wananchi, ambayo yameorodheshwa kwenye rasimu,
yanakinzana na matakwa ya chama hicho hiyo ndiyo sababu,” alisema Kakobe
kwa msisitizo.
Askofu huyo alisema, ikibidi Rais Kikwete
angefanya uungwana kwa kurejea tena kwa wananchi kwa kuandaa hotuba
nyingine ili kuwaomba radhi kwa kuvuruga mchakato huo ndiyo mambo
mengine yaendelee.
“Hata kama yeye ni kiongozi, kama amekosea,
anatakiwa kuomba radhi…lazima awatendee wananchi haki yao kwa kukiri
kuwa yeye ndiye chanzo cha mvurugiko huo ili kuruhusu mchakato wa Katiba
uendelee ili Watanzania wapate Katiba wanayoitaka,” alibainisha Askofu
Kakobe na kuongeza:
“Sasa umefika wakati wa chama tawala kukubaliana
na mabadiliko yanayotokea. Wananchi wa sasa siyo wale wa zamani
wakuburuzwa tu. Siku hizi watu wajanja, watu wanataka kuona maoni
waliyopendekeza yanafanyiwa kazi bila kuweka usiasa ndani wala si
vinginevyo.”
Alisema kuwa juhudi zote za kuunda kamati kwa
ajili ya kufanya vikao vya maridhiano ili kutaka Ukawa warejee bungeni
zimekuwa zikigongwa mwamba kutokana na kukosa uthabiti juu ya hilo.
0 comments:
Chapisha Maoni