KIFO cha ghafla cha mwigizaji na mwongoza filamu za Kibongo, Adam Philip Kuambiana kimeibua mazito ya kutosha, Uwazi limeshika kitu mkononi.
Moja kati ya mazito hayo ni kuwepo kwa madai kwamba marehemu alikula au alilishwa sumu kupitia chakula.
Mwili wa mwigizaji na mwongoza filamu za Kibongo, Adam Philip Kuambiana ukipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kwa mujibu wa rafiki mmoja wa karibu wa Kuambiana aliyeomba hifadhi
ya jina lake, marehemu Kuambiana asingekufa ghafla kama tatizo lilikuwa
vidonda vya tumbo au kisukari, ila kuna sumu iliingia tumboni mwake
kupitia chakula.“Siku ile Kuambiana alikuwa ana pesa, alianza kunywa pombe kuanzia asubuhi lakini pia alikuwa anakulakula kila alipojisikia. Naamini katika kulakula huko ndiko alikumbana na janga hilo,” alisema rafiki huyo.
BAA YAHOFIWA
Mtu huyo wa karibu alikwenda mbele zaidi kwa kudai kwamba ana wasiwasi na baa moja ambayo hakuitaja kwa jina kwamba huenda marehemu alikula hapo kwani alikuwepo kwa muda mrefu siku ya Ijumaa.
“Unajua ninaposema alikula chakula chenye sumu sina maana wahudumu walimwekea sumu kwa makusudi. Ila siku hizi kuna ‘food poison’ (sumu kwenye chakula) ambayo mtu anaweza kujikuta anakula kupitia chakula, soda au juisi bila kujijua,” alisema mtu huyo.
ALICHOSIKIA STEVE NYERERE
Wakati rafiki wa karibu wa Kuambiana akiwa na wasiwasi na sumu, Uwazi lilizungumza na Mwenyekiti wa Bongo Movie Unity, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ ambaye alisema habari zilizoenea ambazo yeye amezisikia ni kuwa marehemu alikunywa dawa (hakusema dawa gani) pia akanywa bia jambo ambalo kama ni kweli alitengeneza sumu mwilini.
Binadamu wanasema mengi lakini mimi nilichosikia marehemu alikunywa dawa halafu akanywa bia zake na ndiyo chanzo cha kifo chake cha ghafla.
“Lakini mimi ninachoamini yule bwana amekufa kwa sababu ya vidonda vya tumbo (ulcers). Lakini pia alikuwa akisumbuliwa na kisukari (diabetes).
“Unajua alipewa masharti asinywe pombe halafu msosi uwe wa uhakika sasa inaonekana kwenye kuyazingatia hayo masharti ndiyo ikawa shida kidogo,” alisema Steve Nyerere.
MKE WA NDOA WA KUAMBIANA AIBUKA
Nje ya Hospitali ya Mama Ngoma, Mwenge jijini Dar, Jumamosi iliyopita ambako wasanii walikusanyika kuuchukua mwili wa Kuambiana na kuupeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili gumzo lilikuwa ‘kumbe Kuambiana alikuwa na mke!’
Ni baada ya mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Janeth Rithe ambaye ni Diwani wa Kunduchi kwa tiketi ya Chadema kufika akiwa analia. Ilibainika kuwa, mwanamke huyo ndiye mke wa ndoa wa Kuambiana na walizaa mtoto mmoja .
UHUSIANO WA MAREHEMU NA STARA THOMAS WAZUA GUMZO
Kuibuka kwa Janeth kuliibua maswali kutoka kwa wasanii mbalimbali wakiwemo wadau wa filamu ambao pia walikuwepo. Wengi walijiuliza ilikuwaje marehemu alitangaza ndoa na mwanamuziki wa Bongo Fleva, Stara Thomas mwaka juzi wakati ana mke wa ndoa?
Wengi walisema huenda walitaka ‘kiki’ ya sanaa kwani licha ya kuanikwa kwa uhusiano wao pia Stara alikuwa akitangaza kutoa albamu yake ya Injili iliyojulikana kwa jina la Nani ni Mshamba?
STARA AZUNGUMZA NA UWAZI
Kufuatia gumzo la uhusiano huo, juzi Uwazi lilimtafuta Stara kwa njia ya simu ya mkononi na kumuuliza kuhusu hilo ambapo alisema:
“Ni kweli tulikutana na Kuambiana na tulipanga kuoana. Lakini kuhusu mke yeye aliniambia alimpa talaka. Kwa hiyo alikuwa huru.
“Hata hivyo, tulipeana muda wa kusomana tabia. Oktoba mwaka juzi (2012) tulitofautiana kidogo tukavunja uhusiano. Tukawa tuko pamoja kwa ajili ya sanaa tu, hasa filamu,” alisema Stara.
MAREHEMU ALIMPIGIA SIMU SAA 2 KABLA YA KIFO
Stara aliendelea kuweka wazi kwamba, Jumamosi ya kifo chake, Kuambiana alimpigia simu saa mbili asubuhi akamwambia anajisikia kuumwa sana.
“Alisema anajisikia kuumwa sana, akakata simu hapohapo. Baadaye nikasikia anapelekwa hospitali, mara nikasikia amefariki dunia,” alisema Stara.
NDUGU WAMKATAA MTOTO
Habari zaidi zinadai kuwa, marehemu alizaa na Janeth mtoto mwenye miaka 6 sasa aitwaye Miriam lakini ndugu wa marehemu wamedai mtoto huyo si wa Kuambiana huku ndugu wa mwanamke wakidai ni wa marehemu.
ANAZIKWA LEO, BAJETI MILIONI 5
Marehemu Kuambiana anazikwa leo Jumanne kwenye Makaburi ya Kinondoni jijini Dar baada ya kuagwa kwenye Viwanja vya Leaders Club.
Marehemu anakwenda sambamba na marehemu Steven Kanumba kwa siku ya kufa (Jumamosi), kuagwa (Leaders Club) kuzikwa (Jumanne) na makaburi (Kinondoni).
Kwa mujibu wa Steve Nyerere, bajeti nzima ya msiba huo ni shilingi milioni tano na Bongo Movie imebeba jukumu la mazishi kwa asilimia 95 kuanzia jeneza, maji siku ya kuagwa Leaders na kaburi.
0 comments:
Chapisha Maoni