Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Dk. Hamisi Kigwangalla, akichangia mjadala bungeni jana.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na wajumbe wa bunge hilo walipokuwa wakichangia azimio la kufanya marekebisho ya Kanuni za Bunge Maalum.Akichangia kwenye mjadala huo, Dk. Zainab Gama alisema kazi ya tume hiyo imeshamalizika na sasa haitakiwi kuendelea tena kuingilia kazi inayofanywa na wajumbe hao.
Dk. Gama alisema itungwe kanuni itakayoruhusu bunge hilo kumuita na kumhoji mtu yeyote atakayelisema vibaya bunge hilo.
KIGWANGALA
Naye Dk . Hamisi Kigwangala, alisema kazi ya Tume hiyo ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Warioba ilimaliza kazi yake lakini bado anashangaa kuona ikiendelea kukosoa kazi inayofanywa na bunge maalum.
“Tume ilishamaliza kazi yake, lakini cha kushangaza kutwa ni kwenye midahalo kwa ajili ya kupotosha na kukosoa kazi inayofanywa na bunge hili, jamani ongeeni na wazee wenzenu muwaambie waache, waambieni muda wao umeisha,” alisema.
Dk. Kigwangala alisema aliwahi kushiriki katika mdahalo na Jaji warioba na alimuhoji ni wapi Bunge maalum la katiba lilipokosea lakini Jaji huyo hakuwa na jibu.
CHEYO
Kwa upande wake, John Cheyo, alisema bunge hilo linaweza kuendelea lakini ni vyema kungekuwa na maridhiano ya pande zote mbili.
Cheyo alisema kusiwe na kuharakishwa kwa Bunge hilo ili kupatikana kwa katiba mpya na badala yake ikibidi baadhi ya vifungu vichukuliwe kwenye rasimu ya sasa na kuboresha Katiba ya zamani.
Alisema kila kitu kinaweza kufanyika ikiwa ni pamoja na kupata theluthi mbili kwa kila upande na kuipitisha katiba hiyo lakini ni vyema kuwapo na maridhiano na aina ya mfumo wa serikali ambayo ni msingi kwa kila kitu.
“Kujadili sura zote na kupiga kura mwisho bado tatizo halijaondoka, tatizo hapa kuna nchi mbili na watunzi wa rasimu wangetupa msingi wa serikali moja au mbili…lakini hatuna hivyo vitu tuna vya serikali tatu tu,” alisema Cheyo.
MIDAHALO YAMKERA SITTA
Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, amevijia juu vyombo vya Habari vinavyorusha midahalo ya Katiba inayoendelea maeneo mbalimbali nchini kwa madai kuwa vimeacha kazi zake za habari na kurusha midahalo.
Kadhalika, ameitaka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kuchukua hatua dhidi ya vyombo hivyo.
Sitta alitoa kauli hiyo baada ya mjumbe, Hamis Dambaya, alimtaka Mwenyekiti huyo kuangalia namna ya kuwazuia wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuendelea kuzungumzia mchakato huo.
Alisema wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wanafanya mambo yanayosigana na Bunge hilo na kwamba Tume hiyo kuendelea kuwahukumu wajumbe hao ni sawa na kuwa na mashambulizi ndani na nje.
"Tume inafanya yake nje na sisi tunafanya ndani, tunamuomba Mwenyekiti azungumze na wazee hawa (Jaji Joseph Warioba) na wenzake waache kulizungumzia suala hili," alisema.
Baada ya mjumbe huyo kumaliza kuongea, Sitta alisema " kuna chombo kimoja cha Habari (hajakitaja) kimeonekana bingwa wa midahalo, kila kukicha wanaonyesha midahalo, na wazungumzaji ni wale wale ndani ya midahalo hiyo," alisema Sitta.
"Serikali inaangalia na kusikia tunaomba ichukue hatua na tunaamini zinachukuliwa, chombo cha habari kimeamua kujiwekea mikingamo na Bunge...serikali inasikia," alisema.
Naye mjumbe Makresia Pawa, alisema mjadala wa Rasimu umefikia katika kujadili kugawana madaraka na kuwasahau wananchi ambao masuala yanayowagusa ni ardhi, maji Maliasili.
Alisema ni vema Bunge likawa na kinga dhidi ya mashambulizi ya nje yanayoelekezwa kwao na kwamba ni vyema kanuni zikapanuliwa na kuwachukulia hatua wana zungumzia masuala ya Bunge hilo nje ya Bunge.
Wajumbe wengine waliendelea kumnanga na kumchambua Jaji Warioba na wajumbe wake huku wakimtaka Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samwel Sitta kuzungumza nao na kuzuia mijadala inayoendelea.
Mjumbe Dk. Hamis Kigwangala, akichangia mjadala wa marekebisho ya kanuni, alisema wajumbe wa Tume hiyo kazi yao ilikwisha na ilivunjwa lakini kila kukicha wanaitisha midahalo na makongamano
"Kazi yao ni kulitukana Bunge Maalum na kusema halina mamlaka ya kubadili Rasimu, wanayojadili hayamo na ha yatokani na Rasimu...hawa wanatakiwa kufanywa nini, kinachofanyika ni upotoshwaji usio na maslahi yoyote kwa umma," alisema.
"Ni mambo ambayo hatupashwi kuyaruhusu yaendelee kutokea, ni nani mwenye mamlaka ya kuwasitisha wajumbe hawa? naomba Mwenyekiti uwaite na kuzungumza nao kiutuuzima, kuwazuia kufanya upotoshaji ni wazee wenzenu naamini watawaelewa, " alifafanua.
"Kazi yao imekwisha, walihurumie hili Taifa watu ache tuandike Katiba, wakati wao (Tume ) wanaandika sisi wabunge tulijua tutakuwa wabunge tuliandika sheria, hatukuingilia mchakato tulijua wanafanya yao tuliwasoma, zamu yao imeisha sasa ni zamu yetu tunaandika Katiba, tunafuata sheria hatujakosea," alibainisha.
"Leo hii wanakusanyana (Tume ) mara kongamano mlimani, kwa wanaharakati, wanajadili na kazi yao ni moja, wamepewa coverage kwenye TV kuliponda Bunge la Katiba kana kwamba hatuna uhalali wowote, maoni yaliyopo hayapashwi kugushwa kama ndivyo kulikuwa hakuna haja ya kutupa siku 70 na kuongeza 60 bali tungekaa wiki moja na kupiga muhuri," alisema.
Dk. Kigwangala alisema kungekuwa hakuna haja ya Bunge, Tume ingepeleka kwa wananchi na kwamba kama Bunge lina mamlaka kamili liachwe lifanye kazi yake.
Alisema wazee hao wameelewa na nchi na wamepewa nafasi nyeti na hiyo ndiyo shukrani yao.
" Kama inashindikana kuweka kwenye kanuni, tuipe nguvu kamati ya uongozi kupendekeza namna bora ya kuwashughulikia hao wanaoendelea kupotisha," alisema.
Alisema kamati ya kanuni ifikirie kutenga kanuni nyingine itakayoleta udhibiti wa wajumbe, kuoendekeza kwa rais kusitisha ujumbe wa watu ambao wamejitoa lakini wanakwenda kupotosha umma.
"Kamati ya kanuni ifikirie kuongeza kanuni nyingine, iipe nguvu kamati ya uongozi mamlaka ya kufikiria ni kwa namna gani mjumbe ambaye anamamlaka ya kuwepo humu na anatakiwa kuwepo, lakini amejitoa, anaendelea na kazi za kutunga Katiba lakini anafanya kazi zake nje ya chombo hiki (Bunge) akiwa nje, tuna namna za kufikia maridhiano na mashauriano iwapo watatofautiana na kufanya uamizi," alisema.
Akijibu hoja hizo, mjumbe wa kamati ya Kanuni, Evord Mmanda, alisema kanuni zinazotungwa na Bunge hilo ni kwa ajili ya kusimamia mijadala ndani ya Bunge na siyo nje ya Bunge.
Kuhusu kutengua au kufuta ujumbe wa wajumbe waliotoka nje, alisema sheria haijaeleza bayana nini kifanyiwe iwapo mjumbe hatahudhuria bali kinachokatiza ujumbe ni kifo pekee.
Alisema Bunge hilo linaunda na makundi matatu ambayo ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya. Muungano wa Tanzania, Baraza kwa Wawakilishi na wajumbe 201 wa kuteuliwa na Rais.
Alisema wabunge na Wawakilishi nafasi zao zinakoma baada ya ubunge au uwakilishi wao kukoma.
EZEKIEL OLUOCH
Mjumbe Ezekia Oluoch, alisema ingawa Bunge hilo limepitisha mabadiliko ya kanuni kwa ajili ya kuwashughulikia wajumbe wanaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ni dhahiri Katiba hiyo haiwezi kupatikana na hata ikipatikana haitadumu.
Oluoch ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT),alisema ili Chama cha Mapinduzi (CCM) kionyeshe ukomavu wake kisiasa ni lazima wajumbe wa bunge hilo wajiridhishe kwanza kuhusu akidi kwa kuzipigia kura sura ya kwanza na ya sita ili kupata picha halisi.
“Hii katiba haiwezi kupatikana na hata ikipatikana haiwezi kudumu kwa sababu yapo makundi saba yanayowagawa wajumbe kisiasa. Nashauri bunge
liibane CCM ionyeshe ukomavu wake kisiasa kwa kuwahakikishia watanzania suala la akidi.Mpaka sasa yanasemwa mambo kisiasa lakini
hakuna uhakika na hata Naibu Katibu Mkuu wao (Mwigulu Nchemba),”alisisitiza Oluoch.
Aliyataja makundi yanayowagawa yanayotishia matumaini ya kupatikana kwa katiba ya Watanzania ni la Magogoni ambalo linasaka urais, dola kivuli, wasio na maamuzi pamoja na kundi la Tumbatu lililopo visiwani Zanzibar.
“Makundi mengine ni kundi la Wasaka tonge ambalo linawajumuisha wajumbe kutoka kundi la watu 201 ambao kimsingi wanahaha kusaka ubunge na ukuu wa wilaya baada ya uchaguzi mkuu. Lakini kundi kubwa zaidi na hatari ni hili la Yohana mbatizaji ambalo limebeba vijana wengi na kundi la Hatimiliki ambalo linafikiri bila CCM hakuna Tanzania, ”alisema.
MWIGULU NCHEMBA
Kwa upande wake Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, ametaka Bunge hilo lisiendelee bila kuhakiki wajumbe watakaoshiriki kwa
kupiga kura ili kujiridhisha ikiwa idadi yao itatosheleza.
Akichangia hoja wakati wa mjadala wa azimio la marekebisho ya kanuni za Bunge hilo, yaliyowasilishwa bungeni na Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge hilo, alisema haitaleta maana ikiwa watatumia muda wote uliotengwa na kushindwa kupata Katiba inayopendekezwa, kwa kukosa theluthi mbili.
“Hata wajumbe ambao hawajafika wahojiwe kwa simu ifahamike ikiwa watafika au la, ili ipatikane idadi kamili ya wajumbe wanaoendelea na kazi hii, isije kufika mwisho tukajikuta hatutoshi kukidhi idadi inayotakiwa kisheria kupiga kura,” alisema Mwigulu.
Alisema siku zinazotambulika kuwa za kazi kwa Bunge hilo zisikomee ijumaa, bali hata jumamosi ili iwe ya kazi kusudi fedha zinazolipwa zitendewe haki.
Michango ya iliyotolewa na Mwigulu bungeni jana, ilitafsiriwa na Katibu wa CWT, ambaye pia ni mjumbe wa Bunge hilo, Ezekiel Oluoch kuwa ni ishara mwanasiasa huyo amepevuka kisiasa.
Imeandikwa na Godfrey Mushi, Editha Majura, Jacqueline Masano na Salome Kitomari
0 comments:
Chapisha Maoni